ARDHI BLOG

HOTUBA YA KATIBU MKUU WA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI, NDG. ALPHAYO J. KIDATA, KATIKA UFUNGUZI WA WARSHA NA MKUTANO WA MWAKA WA TAASISI YA WANATAALUMA YA UTHAMINI, UWAKALA WA MAJENGO NA HAKI ZA ARDHI, USIMAMIZI WA MILIKI NA MAENDELEO YA ARDHI TANZANIA “TANZANIA INSTITUTION OF VALUERS AND ESTATE AGENTS – TIVEA” TAREHE 29-30 JANUARI, 2015, BLUE PEARL HOTEL, DAR ES SALAAM.

 

Ndugu Rais wa TIVEA,
Wajumbe wa Baraza la Utendaji na Baraza la Uongozi,
Wanataaluma Wote,
Mabibi na Mabwana

Awali ya yote, napenda kuwashukuru sana kwa kunikaribisha asubuhi hii kuwa Mgeni Rasmi katika wasaa huu wa ufunguzi wa Warsha na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Taasisi ya Wanataaluma wa Uthamini, Uwakala wa Majengo na Haki za Ardhi, Usimamizi wa Miliki na Maendeleo ya Ardhi. Kama mnavyojua, Wizara yetu ni Wizara mama kwa taaluma nyingi zinazohusika na maendeleo na usimamizi wa ardhi ambazo watu wake wanakutana hapa leo na kesho kwa ajili ya kukumbushana na kujadili mienendo na mustakabali wa taaluma zao.

Napenda kuchukua fursa hii kuipongeza Taasisi yenu kwa kuweza kuendesha Warsha za mafunzo za mara kwa mara. Hili ni jambo la msingi kwa ustawi wa taaluma yoyote, hususani ukizingatia mabadiliko ya haraka ya kitaaluma duniani. Ili kuwafanya wanataaluma nchini kuendelea kuwa sawa na wengine duniani ni vyema kuandaa warsha na mafunzo ya namna hii mara kwa mara.

Ni matumaini yangu kwamba mada zitakazowasilishwa na kujadiliwa hapa leo na kesho zitakuwa ni zile zinazoendena na zinazotoa ufumbuzi wa changamoto mbalimbali mnazokumbana nazo katika utendaji wenu wa kila siku. Nina uhakika kuwa mada hizi zinaendana na hali halisi ya sasa ambapo Watanzania tunatakiwa tuwe na weledi na uadilifu wa hali ya juu katika kutimiza majukumu yetu.

Nimejulishwa kuwa kesho, pamoja na masuala mengine, mtakuwa na Mkutano Mkuu wa mwaka ambapo mnatarajia kujadili mabadiliko ya Katiba ya Taasisi yenu ili iendane na mazingira ya sasa. Mabadiliko haya ni kuweza kuifanya Taasisi kuwa bora zaidi na kuisogeza karibu na wanataaluma wote. Kwa muundo wa sasa wa Taasisi, baadhi ya wanataaluma huona wametengwa. Wengi wa wanataaluma kama vile Maafisa Maendeleo ya Ardhi na Wasimamizi milki huona kwamba Taasisi ni ya Wathamini na Mawakala wa Majengo na Haki za Ardhi pekee. Naaamini ufumbuzi wa suala hili umo ndani ya uwezo wenu, na kama katiba iliyopo haizingatii taaluma zilizobainishwa hapo juu ni wakati muafaka katika mabadiliko mnayotarajia kuyafanya mzingatie na haya.

Mabibi na Mabwana
Nimeelezwa kwamba moja ya changamoto iliyopo mbele yenu hivi sasa ni ufanyaji kazi usioridhisha wa Bodi yenu ya Usajili “National Council of Professional Surveyors (NCPS)”.Kumekuwa na malalamiko mengi kuhusiana na utendaji kazi wa Bodi hususani katika muundo na utendaji wake. Nimesoma kwenye ratiba yenu kwamba suala hili litajadiliwa katika warsha hii pia. Nitaomba mniletee mapendekezo yenu ili tuone jinsi gani tutakavyo saidia kuimarisha taasisi hii. Hata hivyo, naamini suluhisho la kudumu la matatizo mengi litapatikana baada ya Sheria ya Wathamini kupitishwa ambayo iko katika hatua za mwisho kutungwa.

Mabibi na Mabwana
Ningependa kuchukua fursa hii kuzungumzia masuala muhimu ambayo Wizara inakusudia kuyafanya ili kuboresha taaluma ya Uthamini na Uwakala wa Milki.

Kumekuwa na malalamiko kwamba wapo watu ambao siyo wathamini lakini hufanya kazi za Uthamini. Pia yapo malalamiko yanahuyosiana na ukosefu wa maadili kwa upande wa Wathamini, Maafisa Ardhi na hata Mawakala wa Majengo na Haki za Ardhi. Kwa mfano, wathamini wanatuhumiwa kufanya tathmini za nyumba hewa, au kuongeza kiwango cha thamani ya mali kwa kusukumwa na rushwa. Pia ni suala la kawaida jengo moja kuwa na thamani tofauti kuendena na dhumuni la uthamini. Mtu aliyenunua jengo na ambaye kisheria anapaswa kuhamisha haki za msingi na kulipa kodi za serikali hukubaliana na mthamini kukadiria kiwango cha chini cha thamani. Lakini anapotaka kuchukua mkopo benki, thamani ya jengo hilo hilo hukadiriwa juu sana. Masuala haya yanadhalilisha taaluma yenu.

Kwa upande wa Maafisa Ardhi, malalamiko ya wananchi yamekuwa juu ya ucheleweshwaji wa makusudi wa upatikanaji wa huduma ili kutumia mwanya huo kutengeneza mazingira ya rushwa. Kwa upande mwingine, Mawakala wa Majengo wameonekana kuwa wakitekeleza majukumu yao bila ya kuzingatia mwongozo wowote. Kutokana na hili kumekuwa na malalamiko ya wananchi juu ya kuibiwa fedha zao na watu wanaojiita madalali. Madalali pia wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya utakatishaji fedha chafu.

Katika kushugulikia matatizo hayo, Wizara imechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kukamilisha Rasimu ya Sheria ya Wathamini “Valuers’ Act”. Sheria hii itawezesha kuundwa kwa chombo cha kuratibu mwenendo wa Wathamini “Valuers’ Registration Board”. Ni imani yangu kwamba tabia zisizofaa katika uthamini zitakuwa zimekomeshwa kwani Bodi hiyo itakuwa na mamlaka ya kumchukulia hatua yeyote atakayekwenda kinyume na sheria na taratibu.

Bodi hii itatakiwa kufanya utafiti ili kuweza kutoa taarifa zitakazowasaidia wathamini wote kuzitumia na kuweza kuondoa utata wa wathamini tofauti kutoa thamani tofauti kwa mali ileile.

Mabibi na Mabwana
Kwa sasa tuko kwenye mchakato wa kutunga sheria ya kuratibu Wakala wa Majengo na Haki za Ardhi, “Estate Agency Act”. Sheria hii itasimamia usajili wa mawakala. Baada ya sheria hii kupitishwa madalali wataweza kulipa kodi za serikali kwa kipato wanachokipata katika kutoa huduma zao. Kwa sasa madalali wengi hawasajiliwa na chombo chochote na hawalipi kodi, pamoja na kwamba wanajipatia kipato kikubwa katika kazi hizo. Pia, tunataka kuweka mfumo wa wazi katika soko la nyumba ili wananchi waweze kuzipata taarifa za thamani za nyumba kwa urahisi na bila kutumia gharama kubwa.

Sheria hii ya Estate Agency itaweka utaratibu utakaowezesha hata kama mwenye nyumba hayupo, kwa mfano wale waliopo nchi za nje “Diaspora”, itawezekana kwa Wakala kusimamia uuzwaji, au upangishwaji wa nyumba yake bila kuwa na wasiwasi.

Ili kuufanya utungaji wa sheria hii ya Estate Agency kuwa shirikishi, nimeagiza ijadiliwe na wadau wa sekta yetu. Nimeambiwa kuwa rasimu ya sheria hii itawasilishwa na Afisa wa Wizara yangu katika mkutano huu. Nawaombeni mtoe maoni yenu kwa nia ya kujenga na mtuwezeshe kuipelekeka mbele sheria hii ili iweze kuanza kutumika mapema iwezekanavyo.


Mabibi na Mabwana
Wizara pia ipo katika mchakato wa kuiangalia upya sheria ya Utwaaji Ardhi na Kulipa Fidia “Land Acquisition Act 1967”. Sheria hii inajikita katika kujibu malalamiko ya siku zote ya wananchi pale Mamlaka zozote ikiwamo Serikali, zinapochukua ardhi kwa ajili ya maendeleo ya umma. Ninyi Wathamini ndio mnafanya uthamini huo, lakini wananchi mara zote wanalalamika kwamba wanapunjwa au hawakujua hiyo thamani imepatikanaje. Matokeo yake ni kucheleweshwa kwa miradi ya maendeleo.

Kama serikali tunataka ifike mahali ambapo, suala la kutwaa ardhi na kulipa fidia lisiwaache wananchi wakilalamika. Mchakato wa kuipitia upya Sheria ya Utwaaji Ardhi itaangalia pia suala zima la kuwapatia makazi mapya na kuwawezesha kuanza maisha mapya, wale wote ambao ardhi zao zitachukuliwa kwa ajili ya mipango ya maendeleo.Kwa ujumla tunataka kuirekebisha sheria hii kwa kuzingatia “best practice” hapa duniani.

Mabibi na Mabwana
Sasa hivi, Wizara iko kwenye mchakato wa kuuboresha Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Sheria za Ardhi yaani “Strategic Plan for Implementation of Land Laws” – SPILL, ambayo ulianza mwaka 2005, kwa sababu nyingi ikiwemo ukweli kwamba Sheria za Ardhi za mwaka 1999 zimefanyiwa marekebisho na zinatakiwa kufanyiwa marekebisho, kumetungwa sheria zingine kama vile ile ya Mipango Miji, na Mipango ya Matumizi ya Ardhi, zote mbili za mwaka 2007. Lakini pia kuna changamoto mpya, mojawapo ni Mikakati ya Serikali ya KILIMO KWANZA na MATOKEO MAKUBWA SASA, ambayo pia inakuja wakati kuna wawekezaji mbalimbali wanaoitaka ardhi ya Tanzania kwa ajili ya kilimo cha biashara, uchimbaji madini, n.k

Mabibi na Mabwana
Tayari Wizara imefanya kazi kubwa katika utoaji wa hatimilki za kimila (CCROs) katika vijiji kadhaa kama njia ya kuwapa wananchi uwezo wa kukopa na kuendeleza miradi yao ya kujiletea maendeleo. Vyombo kadhaa vya fedha tayari vimeweza kutoa mikopo kwa kutumia hatimilki za kimila ingawa bado kuna vingine bado vinasita kukopesha kwa kutumia hatimilki za kimila. Natoa wito kwa vyombo vyote vya fedha kutozibagua hatimilki za kimila kwani ni hati halali za ardhi ambazo zina hadhi sawa ya kisheria kutumika kama dhamana ya mikopo.

Kama mnavyofahamu, Serikali ina mipango mingi ya kuwawezesha wananchi kuondokana na umaskini. Katika mipango hii, taaluma yenu ya ardhi na uthamini ni ya muhimu sana. Hivyo nawakaribisha kutoa mchango wenu ili taifa letu lipige hatua mbele. Kama kuna suala lolote ambalo mnadhani Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaweza kulifanya ili kuboresha Taaluma yenu na kusukuma mbele maendeleo ya Taifa letu msisite kutushirikisha.

Mwisho, Naamini katika mkutano huu mtajadili masuala mengi yenye manufaa kwa taaluma yenu na kwa taifa kwa ujumla. Nitaomba nipewe muhtasari wa mapendekezo mtakayoyajadili ili tuweze kujifunza na kuyafanyia kazi tukiwa kama sekta yenu mama. Kwenye mkutano huu kuna maofisa wengi kutoka Wizara ya Ardhi, ni imani yangu kuwa watashiriki kikamilifu katika mijadala mbalimbali.

Sasa ninayo furaha kutangaza kwamba Warsha hii imefunguliwa rasmi.

Asanteni sana kwa kunisikiliza!

SALAAM ZA MHE. ANNA KAJUMULO TIBAIJUKA (MB) WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA MAKAZI DUNIANI
TAREHE 6 OKTOBA, 2014.

Mhe. Said Mecky Sadick, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Mstahiki Dr. Didas Masaburi, Meya wa Jiji la Dar es Salaam,
Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam,
Mwakilishi Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa UN-HABITAT
Mwakilishi wa Benki ya Dunia na Wahisani wote wa Sekta
Viongozi wa Benki, Taasisi za Fedha na Mashirika mbalimbali,
Waandishi wa Habari, Wageni waalikwa , Mabibi na Mabwana.


Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani hufanyika duniani kote kila Jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba. Mwaka huu tunaadhimisha siku hiyo tarehe 6 Oktoba, 2014 tukitafakari hali ya makazi katika nchi zetu hususan katika maeneo yenye makazi duni na kupanga mikakati ya kukabiliana na matatizo ya makazi kwa kuhusisha Serikali za nchi wanachama kote duniani, wananchi na wadau wengine.

Chanzo cha maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani ni Azimio Namba 40/202 lililopitishwa mnamo mwezi Desemba mwaka 1985 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Siku hii hutoa nafasi kwa kila Taifa, wananchi na wadau wengine wa makazi kutafakari kila mmoja kwa nafasi yake namna alivyoshiriki na atakavyoshiriki kuboresha hali ya maisha katika miji.

Ndugu wananchi,
Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani huongozwa na Kaulimbiu ya mwaka husika. Kaulimbiu hutuwezesha kutafakari suala husika kwa kina na pia hutupatia fursa ya kujiwekea nafasi na mazingira wezeshi ya kutafuta ufumbuzi wa muda mrefu wa suala husika kwa mwaka huo. Mwaka huu Shirika la Makazi Duniani limetoa kauli mbiu isemayo “Sauti kutoka makazi duni``. (Voices from slums) ambayo inatukumbusha kutumia fursa zitokanazo na ukuaji wa miji kwa ajili ya maendeleo licha ya changamoto zinazoweza kuwepo ili kupunguza umaskini. Inakadiriwa kwamba hapa Tanzania watu wapatao milioni 12, sawa na asilimia 30 ya wananchi wote, wanaishi mijini. Kama miji yetu itaendelea kukua kwa kasi ya asilimia 4.5 kila mwaka, ifikapo mwaka wa 2050 zaidi ya nusu ya wananchi wote hapa nchini watakuwa wanaishi mijini. Idadi hiyo inakadiriwa kufikia milioni 30. Aidha idadi ya miji imeongezeka kutoka miji 31 mwaka 1957 na kufikia miji 337 mwaka 2012. Inakadiriwa kwamba kati ya asilimia 60 na 75 ya wakazi wa mjini wanaishi katika maeneo yaliyoendelezwa kiholela. Hii ni changamoto kubwa kwa wenye jukumu la kuhakikisha kuwa miji inakuwa vitovu vya maendeleo na mahali bora pa kuishi na kufanya kazi kwa wakazi wake.
Ndugu wananchi,
Madhumuni ya siku ya Makazi kufuatana na Kaulimbiu ya mwaka huu ni kama ifuatavyo:
• Kutoa elimu kuhusiana na hali ya maisha katika maeneo ya makazi duni;
• Kubuni mbinu mbalimbali na kuanzisha mchakato wa kihistoria wenye lengo la kulinda kumbukumbu za watu wanaoishi katika makazi duni;
• Watunga sera katika nyanja za miji kuonyesha kwamba mipango ya uboreshaji Makazi Duni inaweza kufikia malengo ya kuwa na hali bora ya maisha kwa wakazi wa maeneo duni na kuwa na matokeo makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa njia ya hadithi za kweli;
• Kubadilishana uzoefu juu ya uboreshaji wa makazi duni miongoni mwa miji na maeneo ya mijini duniani kote;
• Kuchangia kwa mapana mjadala wa sera ambao unalenga masuala ya maisha katika makazi duni mijini;
• Kubainisha masuala ya uundaji wa sera za maendeleo ambazo katika mfumo wa Umoja wa Mataifa, hasa UH-Habitat, unaweza kutoa mchango mkubwa;
• Kutambua na kuwashirikisha wadau muhimu katika majadiliano kuhusu uboreshaji wa makazi duni na uzalishaji wa nyumba za kutosha.

Ndugu wananchi,
Mwaka huu Siku ya Makazi Duniani inalenga kutoa fursa kwa watu ambao wanaishi katika makazi duni au maeneo mengine hatarishi yaliyoko ndani ya mipaka ya miji kupaza sauti zao. Serikali, Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), Sekta Binafsi, Taasisi za Umma
na Taasisi nyingine zinahimizwa kuwafanya wakazi wa maeneo duni kuwa wasemaji wakuu wa Siku ya Makazi Duniani kwa mwaka 2014 kupitia majukwaa mbalimbali ya mawasiliano. Ili kufikisha ujumbe hadithi, picha za video, habari picha, mitandao ya kijamii, mahojiano na simulizi nyingine zitasaidia kampeni hii.

Ndugu wananchi,
Kasi ya ukuaji wa miji ni kubwa na inazidi uwezo wa mamlaka husika wa kuwapatia wakazi wake makazi bora yaliyopangwa, yaliyopimwa na kuwekewa miundombinu na huduma za kiuchumi na kijamii, na hivyo kufanya wananchi wengi kujijengea nyumba katika maeneo yasiyopangwa. Upatikanaji wa makazi bora umekuwa na changamoto nyingi sana hasa pale miji inapokua pasipo kuongozwa na Mipango ya Jumla ( master plans) na ile ya Kina ( detailed planning schemes) na kuifanya miji salama na endelevu kukidhi mahitaji ya watu wanaohamia kutoka vijijini kwa nia ya kutafuta fursa bora za maisha.

Ndugu wananchi,
Sisi wote tunajua kwamba kutozingatia sheria na udhaifu katika kusimamia uendelezaji wa miji, ndiyo chanzo cha miji yetu kukua bila mpangilio na wananchi wengi kumiliki na kutumia ardhi bila kibali. Serikali imekuwa inatunga Sera na Sheria za kusimamia ukuaji wa miji iliyopangwa na kudhibiti makazi holela katika miji yetu. Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995, Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000 na Sheria ya Mipangomiji ya mwaka 2007 zinaelekeza kuwa jukumu la kupanga miji na kurasimisha makazi ni la Halmashauri za Miji ambazo ni Mamlaka za Upangaji. Halmashauri mbalimbali zimetekeleza kazi hiyo kuanzia miaka ya1990 kama ifuatavyo:
• Katika Manispaa ya Dodoma, Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA) imerasimisha maeneo ya Chang’ombe, Mailimbili, Oysterbay, Miyuji South, Medeli East na Mlimwa ambapo zaidi ya wananchi 5,651 walipimiwa na kumilikishwa maeneo yao; Manispaa ya Moshi katika maeneo ya Miembeni, Njoro na Mji mpya wananchi wametambuliwa na kupimiwa maeneo yao na kupewa miliki. Aidha, katika Jiji la Tanga viwanja 956 vimepimwa katika maeneo ya Kwanjeka Nyota, Majengo, Mwangonda na Tangasisi na hatua za kumilikisha zinaendelea na maeneo mingine 10 yameandaliwa mipango ya urasimishaji;

• Katika Jiji la Dar es Salaam Serikali, imewatambua wananchi waliojenga kwenye maeneo yasiyopangwa ili kuongeza usalama wa miliki zao kwa kuwapatia leseni ya makazi. Urasimishaji wa kutambua miliki, kuandaa daftari la wamiliki na kutoa Leseni za Makazi yenye uhai wa miaka 5 ulifanyika mwaka 2004-2007 ambapo jumla ya miliki 274,039 zilitambuliwa kati ya hizo milki 230,000 ziko katika utaratibu wa kutolewa hati miliki na Manispaa zinaendelea kutoa Leseni za makazi katika maeneo yaliyotambuliwa awali. Wananchi 105,726 wameshachukua Leseni za Makazi na wananchi wapatao 1,263 wamezitumia katika Taasisi za Fedha kwa ajili ya kupata mikopo;
• Aidha Urasimishaji umefanyika katika eneo la Hanna-Nasif ambapo jumla ya viwanja 1,423 vimepimwa na wananchi 214 wameshapata Hati za Kumiliki Ardhi;
• Miliki 44,039 katika eneo la Kimara na Mbezi zimeandaliwa Mipango ya Urasimishaji na wananchi wamehamasishwa kuchangia gharama za upimaji na hatimaye watapatiwa Hati kamili za kumiliki ardhi;
• Kupitia Mradi wa Kuboresha Miundombinu kwa Kushirikisha Jamii (Community Infrastructure Upgrading Programme – CIUP) maeneo ya Manzese, Buguruni, Vingunguti, Sandali na Chang’ombe yameboreshwa kwa kuwekewa miundombinu na huduma mbalimbali za kijamii katika awamu ya kwanza. Barabara zenye urefu wa kilomita 18.21 zimejengwa, njia za waenda kwa miguu zenye urefu wa kilometa 9.2 zimejengwa, mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa kilomita 27.44 imejengwa, na taa za barabarani 358 zimewekwa kwa ajili ya kuongeza usalama wa maeneo hayo;
• Awamu ya pili ilitekelezwa katika maeneo ya Mwananyamala kwa Kopa, Kigogo, Vingunguti, Azimio, Keko Mwanga A & B, na Magurumbasi A. Katika maeneo hayo, barabara zenye urefu wa kilomita 20.0 zilijengwa, njia za waenda kwa miguu zenye urefu wa kilomita 8.55 zilijengwa, mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa kilomita 30.6 imejengwa, taa za barabarani 784 ziliwekwa kuongeza usalama katika maeneo hayo. Kwa ujumla zaidi ya wakazi 58,000 wamenufaika na mradi huu;
• Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetambua jumla ya miliki 36,172, jumla ya viwanja 14,821 vimepimwa na hati 6,789 zimeshatolewa kwa wananchi;
• Ofisi ya Rais kupitia MKURABITA imerasimisha makazi na kupima jumla ya viwanja 3,541 kama ifuatavyo; Halmashauri ya Mji wa Babati viwanja 529, Halmashauri ya Mji wa Njombe viwanja 1,003, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro viwanja 1,131 eneo la Kihonda, Tuelewane na Falkland na Halmashauri ya Jiji la Arusha viwanja 878 katika mitaa ya Sakina na Kware;
• Halmashauri ya Manispaa ya Tabora imerasimisha na kupima jumla ya viwanja 649 na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imepima jumla ya viwanja 749 katika eneo la Isoka;

Ndugu wananchi,
Jitihada zinazofanyika ni kidogo kulinganisha na ukubwa wa tatizo la ujenzi holela, hivyo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Halmashauri za miji imeandaa Programu ya Taifa ya Kurasimisha na Kuzuia Ujenzi Holela ambayo lengo ni kuwa na chombo cha kuzuia ukuaji na ongezeko la makazi holela na kuhakikisha kuwepo kwa huduma za kijamii na kiuchumi na kuwapa wenye ardhi na nyumba fursa ya kupata hati miliki ya muda mrefu.
Ndugu wananchi,
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo mijini imefanya juhudi za kuboresha makazi kuunga mkono mikakati ya Kurasimisha Makazi na kuzuia ujenzi holela mijini ili kufikia maendeleo endelevu ya miji. Baadhi ya wadau hao na shughuli wanazozifanya ni kama ifuatavyo:
• Chuo Kikuu Ardhi wamefanya tafiti mbalimbali ambazo matokeao yake yamewezasha kutoa maamuzi katika uboreshaji na uendelezaji makazi kwa ujumla.
• Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) wamefanya tafiti kuhusu upatikanaji na utumiaji wa vifaa vya gharama nafuu vitumikavyo katika ujenzi katika eneo mahalia.
• Wakala wa Maji Safi na Taka (DAWASA) wanatoa huduma ya maji katika maeneo mbalimbali ya makazi kwa kuzingatia zaidi uhitaji wa huduma hii kwa wananchi. Aidha pale ambapo imekuwa vigumu kumpatia kila mmoja huduma hii kutokana na msongamano wa nyumba Mamlaka imeweka ‘water kiosk’ ili wananchi waweze kupata maji safi karibu na makaza yao.
• Asasi ya kijamii ya Center for Community Initiatives (CCI) imefanya kazi ya kuhamasisha na kuwaunganisha wananchi waliohamishwa kutoka Kurasini kupisha mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na kununua eneo Chamazi ambapo hadi sasa wameshajenga nyumba 75 kwa wanakikundi hao. Aidha wanatoa ushauri wa kitaalamu wa ujenzi wa nyumba kwa wale walioathirika na mafuriko na kuhamishiwa Mabwe Pande ambapo kwa sasa wameweza kujenga nyumba (5) tano kwa wakazi hao.
• Taasisi za kifedha mfano Benki ya Azania imekuwa benki ya kwanza kukubali kutumia Leseni za Makazi kama dhamana katika utoaji wa mikopo kwa wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo kuboresha makazi.
• WAT Human Settlements Trust wanatoa elimu na mikopo kwa wananchi wa maeneo duni. Katika eneo la Vingunguti wakazi wamekopeshwa fedha na kuelimishwa namna ya kuzitumia kuboresha makazi yao.
• Asasi nyingine ni kama TAFSUS kwa kushirikiana na UN Habitat inasaidia wakazi wa maeneo duni kwa kuwapatia mikopo ya kuboresha makazi yao. Hivi karibuni nimekabidhi wakazi wa eneo la Manzese hundi zenye thamani ya kati ya shilingi milioni moja na nusu (1,500,000) hadi milioni tisa (9,000,000) zikiwa jumla ya sh. milioni mia moja (100,000,000) kwa ajili ya kuboresha makazi yao.
• Shirika la Nyumba la Taifa limeanza kutekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano wa kujenga nyumba 15,000 nchini ili kupunga uhaba wa nyumba mijini, hivyo kupunguza kasi ya ukuaji wa makazi duni.

Ndugu wananchi,

Napenda nichukue fursa hii kuwashukuru pia wadau wengine ambao wanaunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha makazi duni kwa kutoa elimu na huduma mbalimbali za kijamii.

Ndugu wananchi;

Ninapenda kumalizia ujumbe wangu wa Siku ya Makazi Duniani kwa mwaka huu 2014 kwa kusisitiza kwamba kuwa na miji bora endelevu kwa maisha bora ni jukumu letu sote, Serikali itaendelea kuzijengea uwezo Halmashuri zote nchini ili kutekeleza majuku yao kama mamlaka za upangaji kwa:
• Kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uendelezaji wa miji;
• Kuongeza kasi ya kuandaa na kutekeleza mipango ya maendeleo ya miji na kuhakikisha usimamizi thabiti wa taratibu za miji;
• Kuzuia ukuaji holela wa miji kwa kupanga na kuweka huduma muhimu na kuzuia ukuaji wa miji tandavu;
• Kupima viwanja na kuboresha makazi duni kwa kuweka huduma za msingi za kijamii ili kuinua wananchi kiuchumi na kuboresha maisha yao;
• Kuweka mazingira yatakayowezesha na kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa nyumba bora na za bei nafuu hasa kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini na kati na taasisi za kifedha ziendelee kutoa mikopo na kupunguza riba ili wananchi wengi wa maeneo duni waweze kuboresha makazi yao hatimaye kupunguza umaskini.

Ndugu Wananchi,

Natoa rai kwenu kufuata sheria na taratibu za ujenzi mijini ili kuepukana na hasara na usumbufu wa kubomolewa maendelezo yenu pale Serikali inapohitaji kuendeleza maeneo mbalimbali katika miji yetu hususan maeneo ya pembezoni mwa miji. Aidha kwa maeneo ambayo hayana huduma ni vyema kushirikiana kikamilifu na Serikali kuandaa mipango ya shirikishi ya kuboresha maeneo duni na kutunza vizuri huduma zitakazowekwa ili ziwanufishe wengi na kwa muda mrefu.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

 

 

Home