ARDHI BLOG

TANGAZO KWA WANANCHI WENYE VIWANJA VILIVYOPIMWA LAKINI HAWANA HATIMILKI

 

Serikali imeazimia kuhakikisha kuwa viwanja vyote vilivyopimwa kote nchini vinamilikishwa. Hivyo, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inapenda kuwatangazia wananchi wote wenye viwanja vilivyopimwa au nyumba zilizojengwa kwenye viwanja vilivyopimwa kuwa wafike katika ofisi za Ardhi za Halmashauri husika ili waweze kuandaliwa hatimilki kwa viwanja hivyo. Ofisi za Kanda za Wizara zitasimamia zoezi hili ili kuhakikisha kuwa kila Halmashauri inaandaa hatimilki kwa viwanja vyote vilivyopimwa nchini. Zoezi hili limelenga kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa na milki salama, kuondoa migogoro ya ardhi na kuwawezesha wananchi kutumia ardhi yao kama dhamana ya mikopo kwenye taasisi za fedha.

Timu ya watendaji na wataalam kutoka Wizarani itatembelea Halmashauri mbalimbali nchini ili kuhakikisha kuwa wamiliki wa viwanja vyote vilivyopimwa wanapatiwa hatimilki haraka. Wananchi wote wenye tatizo hili wanatakiwa kufika kwenye Ofisi za Ardhi za Halmashauri zao ili kupata maelekezo zaidi juu ya zoezi hili.

Imetolewa na:

KATIBU MKUU

TAARIFA YA MHE. WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI KWA VYOMBO VYA HABARI.

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI.

TAARIFA YA MHE. WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI KWA VYOMBO

VYA HABARI KUHUSIANA NA ZOEZI LA UBOMOAJI WA MAENDELEZO YA KIVAMIZI.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inalo jukumu la kuhakikisha kwamba ardhi inatumika kwa maendeleo endelevu. Ili ardhi itumike kwa maendeleo endelevu ni sharti wamiliki wa ardhi wenye hati za kumiliki ardhi wenye hati za kumiliki ardhi na wamiliki ardhi kimila, milki zao zilindwe na kuheshimika kwa mujibu wa sheria.

Kwa muda mrefu pamekuwa na wimbi kubwa la migogoro ya ardhi inayosababishwa na tabia ya wananchi wasio na nyaraka za kisheria za kumiliki ardhi, kuingia kwenye viwanja vya wananchi wengine wenye hati za kumiliki ardhi na kuviendeleza kiuvamizi pasipo kuwa na vibali vyovyote vya ujenzi. Utaratibu huu ni kinyumbe cha Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999. Kwa mujibu wa kifungu namba 175 (1) cha sheria hiyo ni kosa la jinai kuingia kwenye ardhi usiyoimiliki na kuiendeleza.

Kufuatia hali hiyo, Wizara inatoa tahadhari kwa Wananchi wote wenye tabia ya kuendeleza viwanja visivyokuwa vyao kuacha tabia hiyo kwa sababu uvamizi wa kiwanja ni kosa la jinai na wahusika wote waliodiriki kufanya hivyo, Serikali itabomoa maendelezo katika maeneo hayo yaliyovamiwa kwa kuwa tu yamefanywa kinyume cha sheria.

Imetolewa na Mhe. William Lukuvi (Mb)
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
27 Februari, 2015

 

TAARIFA KWA UMMA.

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI.

TAARIFA KWA UMMA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi anawatangazia wamiliki wote wa ardhi nchini kuwa, kwa mujibu wa Fungu la 33(1) la Sheria ya Ardhi, wanatakiwa kulipa kodi ya pango la ardhi kila mwaka. Kodi hiyo inapaswa kulipwa katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Halmashauri zote nchini. Muda wa kulipa kodi ya pango la ardhi bila riba unaanzia tarehe moja mwezi wa saba mpaka tarehe thelathini na moja mwezi wa kumi na mbili kila mwaka. Baada ya tarehe hiyo, kodi ya pango la ardhi italipwa pamoja na riba.

Kwa sababu hiyo, wamiliki wote wa ardhi nchini mnatakiwa kulipa kodi ya pango la ardhi na malimbikizo yote ifikapo tarehe 31.03.2015. Ikumbukwe kuwa, kutolipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati ni ukiukwaji wa masharti ya umiliki wa ardhi ambao madhara yake ni pamoja na kunadiwa mali au kufutiwa umiliki wa ardhi.

Kwa muda mrefu Wizara imekuwa ikiwakumbusha wamiliki wa viwanja/mashamba nchini kulipa kodi ya ardhi kwa wakati bila mafanikio. Umiliki wa ardhi unaendana na wamiliki kukidhi masharti ya uendelezaji na umilki wa ardhi. Hivyo basi, baada ya muda uliotangazwa hapo juu kupita, Wizara itawatangaza kwenye vyombo vya habari wamiliki wote ambao watakuwa hawajalipa kodi ya pango la ardhi bila kujali wasifu wao sanjari na kuwachukulia hatua stahiki za kisheria. Hakutakuwa na kumbusho lingine tena juu ya suala hili.

Imetolewa na:

 

Mhe. William V. Lukuvi (Mb.)
WAZIRI WA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA
NA MAENDELEO YA MAKAZI.

 

Home